KUNDI moja la wazee wastaafu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), limeanza kujenga ushawishi wa kutaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, achukue fomu za kugombea urais mwaka 2015, RAI Jumapili limebaini.
Wastaafu hao wanaotajwa kuongozwa na mmoja wa wanasiasa wakongwe aliyepata kushika nyadhifa za juu serikalini, ukiwamo uwaziri mkuu, wanatajwa kwamba, tayari wameshafikisha maoni yao hayo kwa Pinda mwenyewe siku chache zilizopita.
Habari hizo zinaeleza kuwa, wazee hao kwa maoni yao, wanamuona Pinda kuwa kiongozi anayeweza kuwa tiba ya migawanyiko ambayo kwa miaka ya karibuni imekuwa tishio kubwa kwa mustakabali, umoja na mshikamano wa chama hicho.
Hatua ya wazee hao kumtaja Pinda zinakuja wakati tayari CCM ikiwa na majina ya wanasiasa wengine kadhaa ambao majina yao yamekuwa yakihusishwa na urais wa mwaka 2015.
Hata kabla ya jina la Pinda kuchombezwa katika orodha hiyo, majina mengine ambayo yamekuwa yakitajwa kwa muda mrefu kuwa katika mchuano huo wa urais ni ya mawaziri wakuu wawili wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Mbali ya hao, wako wanasiasa wa aina ya January Makamba, Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, Samuel Sitta na Bernard Membe.
Wengine wanaotajwa katika orodha hiyo ya CCM ni Stephen Wasira, John Magufuli na Dk. Harrison Mwakyembe.
Gazeti hili limedokezwa kuwa Pinda ambaye ni muumini wa Kanisa Katoliki, mara baada ya kupokea ujumbe huo aliomba muda ili aweze kutafakari, ikiwemo kufunga Novena ili kupata mwongozo wa kiroho.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka katika vyanzo vya kuaminika ndani ya chama hicho, zinamtaja Cleopa Msuya kuwa miongoni mwa wazee waliochukua hatua ya kumshawishi Pinda kufikiria kuhusu kugombea urais mwaka 2015.
Msuya anatajwa kufanya hivyo akiwa ameongozana na mmoja wa marafiki zake wakubwa wa kisiasa (jina tunalo) ambaye amepata kushika nyadhifa za kiserikali na za kichama (CCM), zikiwamo ukuu wa mkoa na uwaziri.
Akizungumza na RAI Jumapili katika mahojiano mahususi yaliyofanyika nyumbani kwake na ambayo yamechapwa katika gazeti hili ukurasa wa 8, Msuya hakukubali wala kukataa na badala yake akasema hataki kuanza kutaja majina ya watu.
“Niseme tu sisi kama wazee wastaafu kama tunaona kuna jambo haliendi vizuri, tunajitahidi kwenda na hapa nijizungumzie mimi kwamba huwa najitahidi kwenda kuwashauri viongozi husika. Tunajitahidi kufanya hivi,” alisema Msuya na kuongeza:
“Sasa lazima tujitahidi kufanya hivyo katika vikao rasmi, kwa hiyo sisi wastaafu kila mmoja kwa nafasi yake akiona jambo ambalo haliendi vizuri aende kwa mtu husika kupeleka maoni,” alisema Msuya.
Alisema yeye kwa sasa anapeleka sifa za za mtu anayefaa kugombea nafasi ya urais 2015 na kusisitiza kuwa kwa sasa hawezi kutaja majina.
“Niseme na hili la kwenda kuzungumza na viongozi wakuu wa chama, si jambo geni ni jambo la kawaida, nimekuwa nikifanya hivyo. Lakini kusema nimepeleka jina hili au lile hapana, nafasi hiyo tusubiri mwakani ndiyo tutaanza kuzungumzia majina ya watu,” alisisitiza Msuya.
Gazeti hili wiki iliyopita lilichapisha sehemu ya mahojiano ya Msuya, akielezea sifa 16 anazotakiwa kuwa nazo rais ajaye.
Wakati Msuya akisema hayo, kwa wiki tatu sasa gazeti hili limeshindwa kupata majibu ya Waziri Mkuu Pinda, licha ya jitihada za kumfikia kufanyika.
Jitihada hizo ni pamoja na kumfikia mwandishi wake wa habari ambaye licha ya kumtaka mwandishi wa habari wa gazeti hili kuandika maswali yake, lakini ameshindwa kutoa majibu hadi sasa.
Hatua ya vigogo hao kumfuata Pinda imeibua minong’ono ya hapa na pale ndani ya CCM kutokana na baadhi yao kutoridhika na utendaji wake, hasa wa kuwa mzito kufanya maamuzi magumu.
Ni kutokana na hilo, baadhi wamekaririwa wakisema kuwa si kweli kwamba Pinda anaweza kurudisha umoja au kuleta amani ndani ya CCM.
Wenye mtazamo huo wanarejea matukio ambayo yamepata kumgusa Pinda moja kwa moja, akinyooshewa kidole kuhusu utendaji wake ambapo wakati fulani baadhi ya wabunge walitishia kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Ni wakati huo ambao Rais Kikwete alimuokoa kwa kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyowaondoa mawaziri wanane.
Wakati hayo yakitokea mwaka jana, hatari ya kung’olewa Pinda iliibuka tena katika mkutano wa 13 wa Bunge la 10 uliomalizika hivi karibuni.
Waziri Mkuu Pinda pamoja na mawaziri wake wawili; Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. Mathayo David, waliingia matatani kutokana na shinikizo kutoka kwa wabunge lililowataka wang’oke katika nafasi zao kutokana na kushindwa kuwajibika katika matukio ya vifo na baadhi ya watu kujeruhiwa, kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa upande mwingine.
Suala la nani atabeba jukumu la kuiongoza CCM katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015 limekuwa likivuta ushawishi mkubwa ndani na nje ya chama hicho katika miaka ya hivi karibuni, si kwa sababu nyingine yoyote, bali ni kutokana na kustawi na kuimarika kwa upinzani.
Pengine, upinzani ambao umekuwa ukitarajiwa kuwa mkali wakati wa uchaguzi huo wa 2015 ni ule wa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho mwaka 2010 mgombea wake wa urais, Dk. Willbrod Slaa alitoa ushindani mkali kwa Rais Jakaya Kikwete.
Hadi hivi sasa, Dk. Slaa ndiye mwanasiasa anayepewa nafasi kubwa ya kugombea tena urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2015