Wakati kampuni mbili kuu zinazotamba kwa kutoa simu bora bado kutoa simu zao kuu za mwaka 2013, yaani Samsung Galaxy S4 na iPhone 5S/6, kampuni nyingine zote kubwa tayari zimeshatoa simu zao bora za mwaka huu. Samsung inatarajiwa kufanya uzinduzi wa Galaxy S4 jijini New York kiasi wiki mbili kuanzia sasa yaani tarehe 14/03/2013, kwa kawaida Apple hutangaza simu yao mpya kwenye mwezi Septemba. Baadhi ya wadau wa teknolojia na gajeti wanatarajia huenda Apple mwaka huu wakatoa simu mbili yaani iPhone 5S na iPhone 6, ikiwa hii ni sahihi basi iPhone 5S huenda ikatoka mwezi wa nne mwaka huu. 
Kampuni ambazo tayari zimeshatoa simu zao bora za mwaka (flagship device) ni pamoja na Nokia, LG, Asus, HTC, Sony na Blackberry. Tutazipitia simu hizo kwa ufupi na kuzungumzia kivutio kikuu na jambo au mambo ambayo huenda yakakwamisha mauzo mazuri ya kila moja wapo. Pia tutachagua na kuchambua ni ipi bora kuliko zote kwa maoni yetu. Kiujumla kampuni nne kati ya sita hizi zimetumia OS ya Android wakati Nokia peke yao wametoa simu ya OS ya Windows Phone. Blackberry kama kawaida yao hutumia OS yao binafsi ambayo ni ya aina ya QNX, safari hii ni toleo nambari 10.

Ubora na Udhaifu
Blackberry Z10


Sifa ya kipekee ya simu hii ni kwamba ina OS ya aina ya peke yake katika soko yaani Blackberry OS 10 ambayo ni mpya. Udhaifu mkubwa wa simu hii ni kwamba Blackberry OS ina apps kidogo kuliko OS zote, idadi ya apps katika Blackberry World ni 75,000. Ukilinganisha na OS inayoongoza kwa apps yaani iOS ya iPhone ina apps milioni moja kwenye Appstore, hivyo unaweza kuona ni kiasi gani apps zinaweza kukwaza mauzo ya Z10. Pia simu hii ni moja kati ya mbili ambazo hazina prosesa yenye core nne. Ikiwa na rezolushani za chini kuliko simu zote 6, Z10 ndio inayoonekana simu dhaifu zaidi ya zote kiumjula kwa upande wa vianisho vya hardware. Uzuri mkubwa katika eneo hili ni kwamba Z20 ndio simu nyepesi kuliko zote ikiwa na uzito wa gramu 137.5

HTC One
Simu hii inavutia kwa vile ni moja kati ya mbili ambazo zina gamba la alumini (aluminium), pia kwa upande wa software, Android Jelly Bean imevikwa Sense 5.0 na Blink Feed. Pia HTC One ina kamera ya kipekee ambapo imetumia Altrapiksel, katika taarifa yao HTC wameeleza kuwa kamera hii inaweza kuingiza mwanga kwa 300% zaidi kuliko zile kamera za megapiksel. Hivyo ni kamera nzuri katika mazingira ya mwangaza mchache. Pia HTC wametumia prosesa yenye kasi zaidi kuwahi kutumiwa kwenye soko la simu yaani 1.7 GHz yenye core nne. Pia simu hii ina kioo chenye mng’aro kuliko zote mpaka sasa ikiwa na piksel kwa kila inchi moja (ppi) 469. Kwa haraka HTC One inaonekana kuwa na vigezo vingi vizuri katika simu hizi.

LG Optimus G Pro
Simu hii ni kubwa kuliko zote ingawa sio nzito kuliko zote (nzito ni Lumia 920), ina kioo chenye ukubwa wa 5.5” ambapo imeingia kwenye anga za phablet. Pia ina prosesa ni yenye kasi kubwa zaidi kwa sasa kama ilivyo HTC One na itakuwa ni kivutio kikubwa kwa wapenzi wa simu kubwa na kero kwa wasiopenda simu kubwa sana. Simu hii inatarajiwa kuwa mshindani wa simu kama vile Samsung Galaxy Note badala ya simu za kawaida. 






Nokia Lumia 920

Ingawa simu hii imetoka mwezi wa 11 mwaka 2012, hii ndio inayotarajiwa kuongoza mauzo ya Nokia kama simu ya hali ya juu ya kampuni hiyo kwa mwaka 2013. Nokia Lumia 920 haivutii kwa upande wa hardware kwa vile ina prosesa yenye core mbili tu na ndio simu pana kuliko zote kati ya sita hizi, ingawa ni ya pili kwa udogo ikiwa imeizidi Z10 tu. Pamoja na udogo wa Nokia Lumia 920 ndio simu nzito kuliko zote sita. Pia sifa ya kipekee ni kwamba inatuia Windows Phone OS ambayo ina sifa wa kufanya kazi vyema hata simu unapokosa nguvu kubwa ya prosesa au RAM nyingi, kwa upande mwengine Windows Phone OS ina app chache ukilinganisha na Android, wakati Android ina apps laki saba Windows Phone ina apps laki moja na nusu tu. Simu hii pia ina chaji bila ya waya ingawa tatizo kubwa la chaji za aina hii ni kuchaji kwa kasi ndogo.

Sony Xperia Z

Sony Xperia Z ndio simu pekee kati ya sita hizi ambayo haingii maji (water proof), pia ndio simu nyembamba kuliko zote katika mkumbo huu ikiwa na upana wa 7.9 mm. Sony wanaonekana kupania kuipandisha hadhi kampuni yao katika soko la simu na tablet ambapo wametangaza wazi kuwa kwa mwaka huu wanatarajia kuwa simu yao itakuwa moja kati ya simu tatu bora. Katika orodha hii tunaweza kuipa simu hii namba moja kwa vile pia ina kioo chenye mn’garo mkubwa ikiwa na ppi 441 ambapo imezidiwa na HTC One tu.

PadFone Infinity
Infinity ni simu ya tatu katika familia ya PadFone kutolewa na Asus. Sifa kubwa nzuri inayoifanya simu hii iwe tofauti na zote ni kule kuuzwa kwake na stesheni ya tablet, yaani kifaa ambacho unapoitumbukiza simu hii kwenye kifaa hicho hugeuka kuwa tablet. Ni chaguo bora kabisa kwa yoyote mwenye nia ya kununua simu na tablet za android kwa pamoja. Kati ya simu nne za Android za orodha hii Padfone infinity ndio pekee iliyokuwa na Android Jelly Bean 4.2 ambalo ndio toleo jipya kabisa. Zilizobaki zote zinatumia Jelly Bean 4.1.2 toleo la pili kutoka mwisho. Padfone kama HTC One ina gamba la alumini na pia ina prosesa yenye kasi zaidi katika simu sita hizi, ikiwa imekwenda sambamba na HTC One na LG Optimus G Pro. Tablet stesheni ya simu hii ina ukubwa wa 10.1”.
MSHINDI KATI YA SIMU HIZI
  Mimi Ngama nimeipa Ushindi Sony Xperia Z katika orodha hii, Ifuatayo ni mfuatano wa simu hizi kwa ubora na sifa kuu nzuri :

1. Sony Xperia Z - haiathiriwi na maji na ina umbile bora kabisa kati ya hizi. Sony pia wametumia teknolojia ya Bravia kuiboresha simu hii na inarusha video kwenda kwenye TV za Sony bila ya kutumia waya, pia ni remoti ya TV zote za Sony. 

2. Asus PadFone Infinity  - Ni simu na tablet kamili, mtumiaji huokoa matumizi ya sim kadi mbili kwa kutumia simu hii. 

3. HTC One - inaonekana ni yenye ubora kimaumbile (quality) na HTC Sense na Blink Feed ni kivutio kizuri. Na ina kasi sawa na simu mbili za juu kwa prosesa. 

4. LG Optimus G Pro - Ni fablet yenye kuvutia ikiwa na kioo chenye ukubwa wa 5.5”

5. Nokia Lumia 920 - Ina simama kipekee kwa kuwa na OS ya Windows Phone, software yake ya kamera ni kivutio kikubwa.(uzito, unene na uchache wa apps umeiangusha Nokia Lumia 920 kiasi fulani)

6. Blackberry Z10 - Software mpya ya simu hii bado ina bugs tulipoijaribu hivi karibuni, pia uchache wa apps umeiangusha simu hii. Lumia na Z10 ndio simu zilizotumia prosesa zisizo na kasi (dual  core 1.5 MHz) na zilzosalia zote zina quadcore. 

Tunaamini wapo ambao watakuwa na maoni tofauti katika mlinganyo huu, tafadhali toa maoni yako kwenye sehemu ya “comment’ chini ya makala hii, ni ipi orodha yako wewe kwa ubora kati ya simu sita hizi na tupe sababu ya ile uliyoichagua namba moja yako ikiwa si Sony Xperia Z10.

Ningependa kutahadharisha kwamba orodha hii haina maana kwamba simu ya mwisho ni mbaya bali ukweli ni kwamba tofauti ni ndogo mno na zote hizi ni simu za hali ya juu.
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top