KATIKA moja ya mambo yaliyojitokeza katika mgogoro wa uongozi wa Chadema, ni tathmini ya nguvu za aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto dhidi ya kinachoitwa udhaifu wa Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Freeman Mbowe na uongozi wake.

Tathmini hiyo ambayo aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo jana ameiita kuwa ni siri iliyowekwa wazi kwa makosa ya kijinga, imeeleza namna kiongozi huyo alivyoandaa mkakati wa kumuondoa Mbowe madarakani kidemokrasia, kupitia nguvu za Zitto.

“Nani tumuunge mkono kuchukua nafasi ya Mkuu (Mbowe).Utangulizi huo (udhaifu wa Mbowe) unaoonesha kinagaubaga kwamba tunahitaji mabadiliko na hatua iliyofuata ilikuwa ni kuangalia nani anaweza kuleta mabadiliko tunayohitaji. “Ni vema ikazingatiwa kwamba mtu ambaye tungemuunga mkono lazima awe mwenye uwezo mkubwa kuliko tunayetaka kumtoa (Mbowe).

Awe ana sifa za kiuongozi na zaidi sana awe na uwezo wa kupambana na mkuu aliyeko. “Katika kuchunguza ndani ya taasisi (Chadema), tuliridhika kwamba Mtendaji Mkuu Msaidizi (Naibu Katibu Mkuu, Zitto), ana sifa zote tulizozitaja hapo juu ingawa kila mwanadamu ana udhaifu wake.

“Ni dhahiri pia kwamba udhaifu wa Mtendaji Mkuu Msaidizi unarekebika kuliko wa mkuu aliyepo,” umeeleza mkakati ambao Dk Mkumbo amekiri kuuandaa na kusisitiza hajutii kazi hiyo aliyoiita ni ya matamanio ya mabadiliko ndani ya Chadema.

“Nasisitiza tena kwamba siamini hata kidogo kwamba matamanio ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, na kuandaa mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia za kidemokrasia ni uhaini,” alisisitiza Dk Mkumbo alipokutana na waandishi wa habari Dar es Salaam kukiri kupanga kumuondoa Mbowe na uongozi wake madarakani.

Udhaifu wa Mkuu Mbowe anadaiwa na Dk Mkumbo kwa kuondoa kipengele cha Katiba ya chama kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano, ili aongoze kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano.

“Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye athari zisizomithilika kwa taasisi yetu,” alisema Dk Mkumbo ambaye alimuomba msamaha Mbowe kwa kumweka wazi namna hiyo.

Katika uchaguzi mdogo, Kitila anasema matokeo ya Chadema yamekuwa dhaifu na kwamba hiyo ni ishara kwamba mabadiliko yanahitajika.

Alisema kuwa tangu uongozi wa Mbowe uingie madarakani, kumefanyika chaguzi ndogo mara nane na uchaguzi wa wawakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi lakini katika uchaguzi huo, Chadema imeshinda mara mbili tu, sawa na asilimia 25.

“Kwa kifupi ushindi ambao tumekuwa tukiupata katika chaguzi ndogo, haulingani na ukubwa wa hamasa kwa taasisi yetu ulivyo mitaani. Hii ni kwa sababu tumekuwa tukitumia mbinu hizo hizo katika kila uchaguzi. Aidha, tu wepesi mno wa kuridhika na kujisifu kwa mafanikio madogo badala ya kukaa chini na kutafakari kwa kina mahala tunapojikwaa,” anasema Dk Mkumbo katika mkakati wake wa kumng’oa Mbowe.

Ubadhirifu wa fedha Dk Mkumbo anasema hakuna mtu anayejua fedha zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu; yaani mkuu kabisa Mbowe, Mtendaji Mkuu, Dk Willibrod Slaa na Mkuu wa Fedha kwenye taasisi hiyo.

“Kuna hata michango ya watu binafsi kama yule Mtanzania mwenye asili ya Kihindi, (Mustafa Sabodo) hizo nazo hazijulikani zimechukuliwa lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje.

“Kwa kiasi kikubwa mkuu aliyepo anatengeneza mazingira yaleyale ya mwaka 2005 na 2010 ya kutaka chama kiwe hakina fedha ili ikifika wakati wa uchaguzi kimpigie magoti. 
Kisha atatoa fedha bila kumbukumbu zozote na mara baada ya uchaguzi atapeleka lundo la madeni na kudai alipwe fedha aliyokikopesha chama wakati wa uchaguzi,” alidai Dk Mkumbo.

Akifafanua Dk Mkumbo alidai baada ya uchaguzi mkuu wa taasisi (Chadema), baadhi wa wapambe wa mkuu walileta deni kubwa la takribani Sh milioni mia tano wakidai kuwa walikikopesha chama. “Taasisi imewalipa fedha zote hizi kwa muda wa mwaka mmoja. Sasa anatengeneza mazingira hayo hayo kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015,” anasema Dk Mkumbo.

Dk Mkumbo anaendelea kuweka wazi kuwa mkuu wa taasisi bila aibu, amekuwa mnunuzi wa vifaa vyote vya chama nje ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na ambayo haihojiwi popote.

“Huu ni mfano wa wazi wa mgongano wa kimaslahi jambo ambalo ni hatari kwa kiongozi mkubwa wa taasisi kama yetu, inayojitambulisha katika kupinga vitendo vya ufisadi na uvunjifu wa maadili ya uongozi kwa ujumla,” alisema.

Kumpata Zitto “Baada ya utangulizi huo unaoonyesha kinagaubaga kwamba tunahitaji mabadiliko, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuangalia nani anaweza kuleta mabadiliko tunayohitaji. Ni vema ikazingatiwa kwamba mtu ambaye tungemuunga mkono lazima awe ni mtu mwenye uwezo mkubwa kuliko tunayetaka kumtoa,” ameeleza Dk Mkumbo.

Amedai mtu waliyepanga kumweka madarakani ni mwenye uwezo wa kiuongozi na zaidi awe na uwezo wa kupambana na mkuu aliyeko. “Tukileta mtu asiyefahamika sana kwenye mifumo ya taasisi yetu hata kama angekuwa mzuri kiasi gani, hatachagulika na mkuu aliyeko atarudi kwa urahisi na kuendelea kuididimiza taasisi,” ameonya Dk Mkumbo katika mkakati huo.

Katika kuchunguza ndani ya taasisi, Dk Mkumbo anadai waliridhika kwamba Mtendaji Mkuu Msaidizi ana sifa zote walizozitaja hapo juu ingawa kila mwanadamu ana udhaifu wake.

“Ni dhahiri pia kwamba udhaifu wa mtendaji mkuu msaidizi unarekebika kuliko wa mkuu aliyepo.“ Sifa za Zitto “Ni kiongozi anayeweza kuongoza taasisi bila kujenga makundi akijali zaidi kazi ya taasisi kuliko maslahi binafsi. Ameonesha kwa vitendo kwamba hana maslahi binafsi kwa kuwa tumeshuhudia akifanya kazi nyingi za taasisi bila kudai malipo kwa njia ya posho ama vinginevyo,” anaeleza Dk Mkumbo.

Amedai kuwa kiongozi huyo anaheshimika na viongozi wa ndani na nje ya taasisi, jambo ambalo ni la muhimu sana kwa ustawi wa taasisi na kwa yeye kuwa mkuu wa taasisi, wanatarajia wakubwa wengi sana kutoka nje ya taasisi wataamini na hata kujiunga katika kuhakikisha lengo la taasisi linafanikiwa.

“Ni msomi wa kiwango cha juu na mwenye uwezo mkubwa katika kuchanganua mambo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kimichezo, jambo ambalo ni muhimu kwa kuwa ni hatari kuwa na kiongozi asiye na ujuzi wa kutosha kwenye masuala kama hayo. Ndani ya taasisi anakubalika kwa makundi yote ya vijana, wazee na akina mama,” alieleza Dk Mkumbo.

Amedai uelewa wa kiongozi wanayemtaka wa mambo ya kiuchumi ni muhimu kwa taasisi kwa sasa kwa kuwa taasisi inahitaji kuja na vyanzo vipya vya mapato ikiwa inahitaji kufanikiwa. “Mkuu aliyepo si kwamba ameishiwa bali hana mbinu za maana za kuiimarisha taasisi kimapato kwa ajili ya malengo yake ya mbele.”
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top