Hayati Steve Jobs alitoa fikra katika mwaka 2007 kwenye uzinduzi rasmi wa iPad ya kwanza, alisema hayati Jobs kwamba tunaingia katika kipindi cha kompyuta za tablet na kompyuta za meza (desktop PC) zimeanza kapitwa na wakati, bila ya shaka yoyote Jobs alikuwa anasema kweli. 

Lakini pamoja na ubunifu, uzoefu na uwezo mkubwa wa uongozi aliokuwa nao Jobs, alichoshindwa kufikiri ni kwamba wabunifu (designers) watachukua yaliyomo kwenye kompyta za tablet na kuyaleta kwenye Komputa za Meza (Desktop PC). Bila ya shaka yoyote hichi ndicho walichokifanya wabunifu wa Lenovo Ideacentre Horizon. 

Unapoitoa kick stand na kuisimamisha Ideacenter Horizon ni Desktop ya kawaida inayotumia Windows 8 Pro. Vimbwanga vya desktop hii vipo kwenye mambo mawili makubwa; kwanza unapokunja stand yake na kuilaza chini na pili ni desktop yenye betri hivyo inaweza kutumiwa kwa muda wa masaa walau mawili bila ya kuchomeka kwenye umeme. Huenda hii ikawa ni desktop ya kwanza kuwa na betri.

Vielelezo vya desktop hii ni kama inavyotarajiwa desktop ya leo; ina diiplay yenye ukubwa 27”, display ina uwezo wa multitouch na rizolushani za HD kamili yaani 1920x1080, display hiyo pia ina uwiano wa 16:9 widescreen. RAM ya Ideacentre Horizon ni 8GB DDR 3 na huku ikiwa na disk ya ukubwa wa 1TB. Lenovo Ideacentre Horizon pia ina kibodi na mouse zisizo na waya (wireless).

Ideacentre Horizon bado haikuanza kuuzwa rasmi, hata hivyo Lenovo waliifanyia uzinduzi rasmi katika maonyesho ya CES huko Las Vegas mwezi uliopita na kompyuta hii ilishinda tuzo ya gajeti bora katika maonyesho hayo. Maonyesho ya Consumer Electronic Show (CES)  yanajumuisha kampuni nyingi kubwa zinazotengeneza desktop za kisasa kama vile Samsung, Asus na HP. 

Lenovo wameahidi kuwa itakapokuwa tayari kuingia madukani Ideacentre Horizon itauzwa pamoja na vikolombwezo (accessories) vitatu maalum kwa ajili ya kuchezea game, na pia itakuja na game zinazohitaji kuchezwa wakati kompyuta hiyo imelazwa chini mfano wa linavyowekwa draft. Mbali na games kompyuta hio itakuwa na software na apps mbali mbali za kuitumia ikiwa imelazwa chini, ni wazi kompyuta hii inafanya lile wazo la Microsoft kutengezwa Surface kwa ajili ya matumizi ya kila siku kuwa ni ukweli unaowezekana.

Ingawa Lenovo hawakuweka wazi ni lini hasa kompyuta hii itaingia madukani lakini mauzo yanatarajiwa kuanza kabla ya kumalizika kwa mwaka huu. Pia bei halisi haikutajwa lakini kwa makisio na uzoefu wetu Ideacentre Horizon itauzwa kwenye anga za kiasi cha shilingi za Kitanzania baina ya milioni mbili hadi milioni tatu. Huu bila shaka ndio mwanzo wa mapinduzi ya Kichina katika teknolojia na gajeti. 
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top