Google ni ulimwengu wa uvumbuzi wa bidhaa na majaribio ya teknolojia, katika baadhi ya mawazo na uvumbuzi ambao Google wanaendelea kufanyia kazi kuna mambo ambayo sio ya kufikirika, gari inayojiendesha na kompyuta ya kuvaa kama miwani ni miongoni mwa teknolojia hizo, kwa mtazamo wa haraka unaweza kudhani kuwa itachukua miaka zaidi ya 10 Google kuweza kuziuza bidhaa hizo kwa watu wa kawaida.
Ukweli ni kwamba Google imeshatangaza kuwa Google Glass itaanza kuuzwa mwaka huu wa 2013. Google Glass ni kompyuta ambayo huvaliwa kama miwani na ina uwezo na matumizi mbali mbali kama vile kurekodi video na kupiga picha. Katika ongezo jipya la Google Glass ni kwamba kompyuta hiyo itaweza kutumia amri za sauti (voice command), kuanzisha amri ya sauti unatakiwa kuiambia miwani hiyo “OK Glass” na miwani itaanza kukusikiliza unataka ifanye nini kabla ya kuipa amri kama vile “record video”. Pia Google wameonyesha baadhi ya matumizi ya miwani hiyo ambayo ni ya kawaida kabisa mbali na yale ya kuchupa na parashuti kutoka kwenye ndege. 


Matumizi hayo ni pamoja na kurekodi video na kupiga picha wakati wa kuendesha gari, unapocheza tenis na wakati wa kupanda mlima, pia Google imeonyesha matumizi ya Miwani  kwa wapanda pembea na wacheza muziki. Miwani hii huenda ikatufanya Waswahili wengi zaidi kuamua kuupanda Mlima wa Kilimanjaro. Pia Google glass itaweza kutoa taarifa kama vile urefu wa barabara unayotembea, ni wakati gani ndege inatarajiwa kutua uwanjani, kutafsiri maneno kutoka lugha moja kwenda nyingine na kukwambia umesimama mtaa gani na hata kukuelekeza njia. Kwa kifupi Google wanaelekea kuipa miwani hiyo uwezo wa “Google Now” ambayo ni search engine inayotumia maneno.




Google tayari imeanza kuwauzia miwani hiyo watengeneza apps (developers) ili waweze kuanza kutengeza apps za miwani hii kwa matumizi mbali mbali. Miwani hiyo itawagharimu developers jumla ya $1,500.00, kwa miwani moja ambazo ni sawa na fedha taslimu za Kitanzania 2,451,000. Google pia imethibitisha kuwa miwani hiyo itakuwa na Apps za simu na tablet za iOS na Android ili kuweza kushirikiana na gajeti hizo katika utendaji wa mambo mbali mbali kama vile ku-send message.


Ingawa teknolojia hii ni mapema mno kujua itakuwa na uwezo na matumizi ya aina gani hasa mbali na haya machache tuliyoyaeleza, wengi miongoni mwa developers wanaelekewa kuvutiwa nayo kwa kiasi kikubwa. Google pia imeanzisha mashindano kwa watu binafsi kuwaandikia twitter au Google+ kueleza ni jinsi gani miwani hii itatumika. Miongoni mwa masharti ya shindano hilo ni kuwa maneno yasizidi 50, video isizidi sekunde 15, picha zisizozidi 5 na utumie hashtag #ifihadglass. Kisha unatakiwa ufuatilie Google+ (+ProjectGlass) au Twitter (@projectglass) na Google imeahidi kujibu direct message kwa washindi. Zawadi kwa washindi ni kuwa kupata nafasi ya kuinunua miwani hiyo mapema, hivyo ukishinda uweke tayari T Sh. Milioni mbili na nusu.
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top