Uvumi na minong’ono ni mambo ambayo hayaachani na kampuni ya Apple yenye makao makuu yake huko  Cupertino. Baada ya uvumi kwamba Apple wangetoa televisheni mwaka huu kuanza kufifia, sasa hivi kuna minong’ono kwamba kampuni hiyo itatoa saa ya mkononi yenye kutumia iOS. Bloomberg imetangaza kwamba kampuni hiyo inatatoa saa ambayo wameipa jina la kubuni la iWatch mwaka huu, ambapo imeripotiwa kwamba Apple tayari ina wafanyakazi karibu 100 wanaoshughulikia gajeti hiyo.

iWatch inasemekana kuwa itakuwa na uwezo wa kushirikiana na gajeti za Apple zinazotumia iOS hivyo kwa kutumia saa hiyo unaweza kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi (SMS), kusikiliza muziki, kuseti miadi kwenye kalenda au kuitumia kama pedometa, kifaa ambacho ni muhimu kwa wanamichezo mbali mbali. Iwapo saa hiyo itatoka basi itaboresha usalama katika maeneo yenye matatizo ya uporaji wa simu kwani hutakuwa na haja ya kutoa simu yako wakati umevaa saa hiyo ili kupiga simu au kufanya matumizi mbali mbali, ingawa tayari unaweza kufanya hivyo kwa kutumia huduma ya app ya Siri na earpods.


Apple ambayo inahitaji gajeti mpya ili kuweza kunyanyua tena thamani ya hisa zake ambazo tangu mwaka jana zimekuwa zikiteremka thamani, imeelezwa kuwa itaweza kupata faida kubwa katika biashara ya saa kuliko televisheni. Kwa mujibu wa mchambuzi wa City Group Bwana Oliver Chen amedai Apple itaweza kuongeza jumla ya $6 bilioni  katika mapato yake iwapo bidhaa hiyo itakubalika na watumiaji gajeti za iOS yaani iPad, iPhone, iPod Touch na Apple TV. 

Uvumi huu unazidi kupata nguvu kwa vile miongoni mwa haki miliki 79 mpya zilizosajiliwa na kampuni ya Apple zipo zinazohusiana na saa ya mkononi, pia itakumbukwa kuwa iPod Nano toleo la mwaka 2010 ilikuwa inaweza kutumika kama saa ingawa iPod Nano hiyo haikuwa inatumia iOS. Vile vile saa hiyo inatarajiwa kuwa na sensa viunganishi mbali mbali kama vile bluetooth, akselerometa na GPS.

Hivi karibuni kumekuwa na gajeti mbali mbali za kuvaa mkononi ambazo zimekuwa zikiuzwa kwa $100 au zaidi, gajeti hizo ni kama vile Nike Fuel Band na Fitbit Zip Wireless, bila ya shaka hivi vimewapelekea Apple kuona kwamba kuna nafasi kubwa ya wao wenyewe kutoa gajeti kama hizi ambapo ikitumia iOS itakuwa na muingiliano mkubwa zaidi na simu, tablet pamoja na iPod zao. 

Huko nyuma Apple ilikuwa ni kampuni ambayo inasifika kwa kuweza kuhifadhi siri za gajeti zao mpya hadi inapofikia uzinduaji rasmi, hivi karibuni gajeti mbali mbali zimekuwa zikivuja na kujulikana habari zake kabla ya Apple kuzitangaza rasmi, mfano mzuri ni pale picha ya iPhone 5 iliposambaa mitandaoni kabla ya simu hiyo kutangazwa na kutolewa rasmi. 

Iwapo saa hii itatolewa basi huenda ikaleta mapinduzi makubwa katika biashara ya saa. Biahsara ambayo imefifia kwa kiasi kikubwa kwa vile watu wengi hawaoni tena umuhimu wa kuvaa saa kutokana na simu zao kuwa na uwezo wa kuwajulisha wakati. Itakuwa ni faraja kwa kampuni zinazotengeneza simu kwani soko litaimarika lakini pia itakuwa ni changamoto kubwa kwa wazalishaji hao kuweza kuinua viwango vya saa zao na kuifikia iWatch. 
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top