Ukizungumzia
kompyuta za mezani, Fusion Leviathan ni mashine ambayo haina mpinzani
kwa sasa katika kasi na nguvu. Hapa hatuzungumzii kupendeza kama kule
kwa gajeti za Apple, tunazungumzia uwezo wa kompyuta kupiga mzigo na
kuwa na ufanisi wa kila namna kwa matumizi ya kompyuta ya leo na hata
miaka 20 ijayo. Kabla ya kueleza vielelezo vya kompyuta hii, tunatabiri
kwamba kompyuta za Apple ambazo ni kompyuta za urembo labda zitafikia
kasi na uwezo wa kompyuta hii mwaka 2020, weka msisitizo kwenye neno
LABDA.
Kompyuta hii
imetengenezwa na kampuni isiyo na umaarufu mkubwa inayojulikana kama
Chillblast iliyoko Uingereza, taarifa za kompyuta hii ni kwa mujibu wa
mtandao rasmi wa Chillblast na jarida la Tech toleo la wiki inayoanzia
tarehe 28/03/2013. Prosesa ya Fusion Leviathan ni Intel Xeon yenye koo
(core) 12, ikiwa na jumla ya kasi ya 55.2 Ghz kwa pamoja. Hivyo kasi ya
koo hizo ni 4.6 kwa kila moja wapo. Mashine hii ina RAM kiasi cha 48
GB, hata hivyo ina slot za kutosha za kuiongezea RAM hadi kufikia 768
GB.
Huu ni wazimu kwa sababu
hakuna anayehitaji nguvu ya namna hii katika shughuli yoyote ya
desktop, hivyo hii ni kompyuta iliyoutangulia wakati kwa muda mrefu
sana. Chillblast walitakiwa waitoe kompyuta hii miaka 15 ijayo. Disk ina
ukubwa wa 21 TB, kwa waliozoea GB zidisha 21 mara 1024, hivyo ni 21,504
GB. Hii unaweza kutumia umri wako wote bila ya kuijaza na sijui
utawezaje kuzimudu (manage) data za namna hii.
Bei ya kuanzia ni
$2,499. Hata hivyo utakapochagua nini unataka uwekewe kwenye kompyuta
hii bei inaweza kufikia $26,000 bila ya kupata taabu sana. Hivyo
kompyuta hii sio tu ina nguvu bali bei nayo si ya kawaida ukizingatia
kwa bei ya $26,000 unaweza kupata gari ya maana ikiwa na maili 0, yaani
mpya kabisa. Bila ya shaka yoyote Chillblast wameitengeneza kompyuta hii
kwa ajili ya watu wenye ugonjwa (addiction) wa kompyuta na wenye fedha
ya ziada ambayo haina kazi. Yaani wale ambao pesa sio tatizo, tatizo ni
matumizi.
Chillblast pia
wanatengeza kompyuta mbali mbali zenye nguvu kubwa kwa bei nzuri,
mashine kama vile Silverstone, Fusion 7 na Fusion Thunderbird. Ingawa
hizi hazina nguvu kama ya Fusion Leviathan lakini itazizidi kompyuta
nyingi tu za hali ya juu, na pia unaweza kuipata kwa bei nafuu sana
ukilinganisha na iMac ya mwaka 2013. Chillblast wanafanya biashara kwa
mtindo wa kupokea oda kwanza. Baada ya kutoa oda huchukua si zaidi ya
siku 10 kukujengea kompyuta yako.