Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefungua milango kwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, katika harakati za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kimesema wanaombeza kwa madai kwamba rushwa anayoipigia kelele iliasisiwa wakati akiwa madarakani, hawalitakii mema taifa.

Kauli ya kumkaribisha Sumaye kujiunga na Chadema ilitolewa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, juzi muda mfupi baada ya Sumaye kumaliza hotuba yake wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kanisa la Lole la Usharika wa Mwika, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Hatua ya Mbowe kumkaribisha Sumaye kujiunga na Chadema inafuatia kauli aliyoitoa Waziri Mkuu huyo mstaafu wiki iliyopita kwamba mahasimu wake kisiasa ‘wanampakazia’ kwamba yeye ni maskini wa kutupwa, hivyo hana uwezo wa kuwapa fedha wanaomuunga mkono katika kupinga rushwa ya uchaguzi, ufisadi na aina nyingine ya uovu kwa jamii ya Watanzania.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu mstaafu (Sumaye), kama nilivyokwisha tangulia kukuomba radhi, huko ulipo ni pagumu, karibu kwetu kwa sababu sisi tunakemea rushwa wazi wazi, tena bila ya kificho, tumekemea rushwa siyo leo, siyo jana. Tuko tayari kufanya kazi na wewe kwa sababu unakemea rushwa, tunakupongeza na karibu sana,” alisema Mbowe mbele ya viongozi mbalimbali wa kisiasa na dini akiwamo Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Askofu Dk. Alex Malasusa.

Mbowe alisema kwamba maneno aliyozungumza Sumaye ameyatafakari kwa kina na kujiuliza maswali mengi kwa kuwa maneno hayo siyo mepesi sana kuyasikia hasa kwa viongozi ambao wamekuwa na mamlaka ya kikatiba kuwaongoza Watanzania.

Alisema kuwa hoja ya rushwa inayotolewa na Sumaye, ni ya msingi sana na haki katika taifa la Tanzania ni bidhaa adimu na kwamba wanaotetea haki wengi wao huipata kwa gharama ya maisha yao.

 “Kwa watu ambao tuko katika active politics (siasa hai), tunaona namna siasa zinavyobadilika na kuwa ni mambo ya kutishia uhai wa watu. Wenzetu viongozi wa Kanisa mtusaidie kuomba ili tusije tukajenga misingi ya kulipasua taifa hili kwa itikadi ya vyama vya siasa,” alisema na kuongeza:
 
“Haya ni mambo ya kupita na Mheshimiwa Sumaye siasa ni kazi ya kupita kesho CCM inaweza isiwapo na Chadema ikawapo…njoo sasa Chadema.”

KAULI YA SUMAYE
Hata hivyo, baada ya ombi la Mbowe, Sumaye hakujibu lolote zaidi ya kutikisa kichwa na kutabasamu.

Sumaye, alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana kuhusiana na kauli ya Mbowe, alisema yeye ni mwana-CCM halisi, hivyo ataendelea kubaki ndani ya chama hicho daima kama mwanachama mwaminifu.

“Kwenye vyama vya siasa, hakuna kualikana, ukijisikia na wakati ukifika unakwenda, Mbowe kazungumza vile kwa kuwa amejisikia kuzungumza mbele ya hadhara ila sina mpango wa kuhamia Chadema,” alisema Sumaye.
 
Kuhusu uwajibikaji wa kibunge, Mbowe alisema wawakilishi wote wa wananchi, mwezi ujao watakwenda kuanza Bunge la Katiba ambalo litachukua miezi mitatu na kwamba kuna mambo mengi ambayo yako gizani mbele yao, hivyo wanaliomba Kanisa lisikae mbali kushiriki nao katika hatua zote za kiukombozi.

Kwa nyakati tofauti akiwa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Kanisa la Visitation Maonano, Parokia ya Mawela katika Jimbo Katoliki la Moshi na hafla ya uzinduzi wa Kanisa la Usharika wa Lole-Mwika wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT mwishoni mwa wiki, Sumaye alisema kuwa hivi sasa rushwa na matumizi makubwa ya fedha za kuwanunua wapigakura, vinataka kuwa utaratibu halali wa kuwapata viongozi kuanzia ngazi za vijiji hadi urais.

“Ukikemea rushwa tu basi utapachikwa sababu nyingi zisizohusika ikiwamo ya kugombea urais mwaka 2015. Nasema katika hili suala la kugombea au kutogombea urais si sababu. Vita yangu dhidi vya rushwa si ya leo,” alisema. 
 
CHANZO: NIPASHE 
 
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top