Baada ya juzi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika kuwaeleza wanahabari kuwa waraka uliochapishwa katika magazeti na mitandao ya kijamii, siyo halisi, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba amejitokeza na kuutetea huku akidai kwamba huo unaodaiwa na uongozi kuwa ndiyo halisi umeghushiwa.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alivuliwa uongozi pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwigamba kutokana na madai ya kuandaa waraka huo ambao Chadema kimesema ulikuwa unaeleza mbinu za uasi za viongozi hao ambazo zingetumika wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo ni kinyume na katiba, sheria na itifaki zake.
Katika tamko alilotoa jana, Mwigamba alidai kwamba
kuna njama zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa Chadema ili kuubadili waraka halisi wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ kwa lengo la kupoteza maana yake, huku akisisitiza kuwa waraka halisi hauna tatizo lolote.
Katika madai yake, Mnyika alisema waraka huo unaosambazwa na kuchapishwa, si ule uliowasilishwa na kujadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu na kuahidi kuutoa waraka halisi ambao una mambo makubwa na mengi zaidi.
“Waraka utakaotumika katika mashtaka yao siyo huo. Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa katika Kamati Kuu ambao una mambo makubwa na mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka halisi,” alisema.
Hata hivyo, jana Mwigamba alisema waraka halisi ni ule ambao upo katika kompyuta mpakato (Laptop) aliyonyang’anywa na wanachama wa Chadema, Oktoba 25, mwaka huu, katika mkutano mjini Arusha.
“Waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ni sahihi neno kwa neno kama nilivyousoma katika magazeti ya jana (juzi), pamoja na nakala iliyopo katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums.”
Aliongeza: “Ili kuthibitisha kwamba waraka ule ndiyo wenyewe, nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye kompyuta yangu kwani waraka huo uliibwa kutoka katika kompyuta hiyo ambayo nilirudishiwa baada ya wao kuikagua na kukuta waraka huo halisi.”
Mwigamba alisema waraka wake unatofautiana kwa kiasi kikubwa na ule ambao Chadema kinasema kuwa ndiyo halisi: “Lissu na wenzake wana mpango wa kuuchakachua waraka huu, lakini wamekwama.”
Alisema kuandaa waraka huo siyo uhaini kama ambavyo imekuwa ikielezwa na viongozi wa Chadema na kusisitiza kuwa ni waraka wa kusaka ushindi katika uchaguzi halali ndani ya chama hicho uliopangwa kufanyika Desemba mwaka huu na baadaye kusogezwa hadi Juni mwakani.
“Wakati wa uchaguzi si ajabu kuwepo kwa wanachama wanaounga mkono wagombea tofauti. Nimekuwa karibu na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa miaka mingi, najua hata yeye ana mikakati na wanaoshiriki mkakati wake ni Lissu na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema,” alisema.
Alisema anashangazwa kwa kitendo cha Chadema kuusambaza waraka huo, wakati ulikuwa ni mpango wa siri kati yake, Dk Kitila pamoja na mtu mwingine anayetajwa kwa jina la M2.
“Baada ya kugundua madhara ya kusambaza ovyo waraka huo, sasa wameamua kuukana, waraka wangu ni sahihi na unaeleza ukweli. Binafsi nimefanya kazi ofisi ya makao makuu ya chama kama Mhasibu Mkuu ningeweza kuanika mengi lakini sijafanya hivyo kwa masilahi ya chama,” alisema na kuongeza:
“Tunatambua kwamba viongozi wetu wanamchukia Zitto na tangu siku nyingi walipanga kumfukuza. Nawashauri watafute sababu nzuri za kumfukuza uongozi na hata uanachama. Zitto hahusiki na mkakati huu pamoja na kwamba alikuwa ndiye mhusika mkuu, alikuwa hajui lolote.”
Jumamosi iliyopita, mama yake mzazi Zitto, Shida Salum ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema waraka huo ulikuwa umeongezwa maneno.
“Hata ule waraka uliongezwa maneno baada ya baadhi ya wanachama kumpora Mwigamba `laptop’ yake alipokuwa mkoani Arusha katika kikao cha Chadema,” alisema bila kutaka kufafanua ulibadilishwa vipi, licha ya kuwataja kwa majina waliohusika kuubadili wakiwamo wabunge wawili wa chama hicho na viongozi wa ngazi za juu.
Sitoki Chadema
Kuhusu hatima yake ndani ya Chadema, Mwigamba alisema hana mpango wa kuondoka hata baada ya kuvuliwa uongozi, huku akisisitiza kuwa hakusudii kuomba radhi kutokana na kuandaa waraka huo.
Alisema hakusudii kuhama kwa kuwa ana historia ndefu na Chadema na anaamini kuwa ndicho mkombozi wa Watanzania.
“Nimekuwa kiongozi wa kata, wilaya, mkoa hadi taifa. Nimetumia muda wangu mwingi na hata kuhatarisha maisha yangu kwa ajili ya chama hiki, siwezi kuondoka kutokana na tofauti za kimitazamo na viongozi wangu,” alisema.
Mwigamba, ambaye alikuwa mfanyakazi katika Mahakama ya Kimataifa inayosikiliza Kesi za Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) na baadaye kujiondoa ili ajikite kwenye siasa, alisema ana imani yanayotokea sasa katika chama hicho yatapita salama.