KESI inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, ya kutuhumiwa kukutwa na simu gerezani, imeshindwa kuendelea kusikilizwa kutokana na shahidi kutokuwepo mahakamani.
Kesi hiyo ambayo inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilishindwa kuendelea kutokana na shahidi wa upande wa Jamhuri kuwepo katika usimamizi wa mitihani ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Airwing, Dar es Salaam.
Liyumba alipanda kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza shauri hilo, ambalo lilitajwa kwa kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri.
Wakili wa Serikali, Peter Sekwao alidai kuwa shahidi ambaye alitakiwa kuja kutoa ushahidi wake, anasimamia mitihani ya taifa ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Airwing.
Hakimu Mmbando aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 26, mwaka huu.
Liyumba anadaiwa kukutwa na simu hiyo alipokuwa gerezani akitumikia kifungo cha miaka miwili, alichohukumiwa na Mahakama ya Kisutu, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka katika ujenzi wa majengo pacha ya BoT.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Liyumba anadaiwa kutenda kosa hilo, Julai 27, mwaka jana, akiwa mfungwa katika gereza la Ukonga.
Inadaiwa alikutwa na simu aina ya Nokia 1280 nyeusi yenye laini namba0653004662 akiwa nyuma ya tangi la maji lililopo karibu na pampu ya maji kwenye gereza hilo.
---Habari Leo