CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk. Kitila Mkumbo, ni waongo na wazushi.

Katika kikao chake cha dharura kilichokutana jana, ikiwa ni siku moja baada ya Zitto na Dk. Kitila kuzungumza na waandishi wa habari, Kamati Kuu ya chama hicho, imesema taarifa zilizotolewa juzi na Zitto na Dk. Kitila kwa waandishi wa habari ni za uongo.

Akizungumza na RAI, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema baada ya Kamati Kuu kupitia taarifa ya Zitto na Dk. Kitila, imebaini kuna upotoshaji na uongo mkubwa ambao unahitaji kutolewa ufafanuzi.
  
 
Hata hivyo, Makene alishindwa kufafanua ni uongo upi uliopo kwenye taarifa zilizotolewa na Zitto na Kitila.

Alisema Kamati Kuu, ilikutana jana kwa dharura na kutafakari taarifa hizo na kuamua kuzitolea ufafanuzi leo hii.

Katika mkutano wa leo, Kamati Kuu ya Chadema itakutana na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi wa kauli za viongozi hao waliovuliwa nyadhifa.

“Baada ya Kamati Kuu kupitia kila kitu, imeamua kesho (leo) mchana itatoa msimamo wa chama kuhusiana na masuala hayo pamoja na masuala ya hali ya kisiasa nchini ilivyo,” alisema Makene kwa ufupi.

Zitto, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, walivuliwa nyadhifa zao ndani ya chama hicho na Kamati Kuu kwa madai ya kufanya uhaini kinyume na matakwa na taratibu za Katiba, kwa kuandaa waraka unaoitwa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’.

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, ameushangaa uongozi wa chama hicho kutangaza kuwavua nyadhifa zao kina Zitto, kabla Baraza Kuu halijaamua.

Profesa Baregu ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema uamuzi wa Kamati Kuu ulikuwa ni sehemu ya mchakato na uamuzi wa kuwavua nyadhifa zao ulikuwa ni wa Baraza Kuu.

“Ninavyoelewa mimi, kuna ngazi za uamuzi ndani ya chama, Kamati Kuu ina mamlaka yake ambayo iko nje ya Baraza Kuu.

“Kamati Kuu ilikuwa na uwezo wa kutoa uamuzi ule, lakini kama sehemu ya mchakato na kuupeleka Baraza Kuu ambalo lina mamlaka ya kuukubali au kuukataa uamuzi huo na kabla ya kuutangaza.

“Nafikiri labda uamuzi wa Kamati Kuu kutangaza kabla ya Baraza Kuu, bado ni sehemu ya mchakato tu, hatua bado hazijachukuliwa, kwani Baraza Kuu linaweza kuyabadili maamuzi ya Kamati Kuu,” alisema Profesa Baregu.

Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa Katiba, Kamati Kuu ilifuata taratibu zilizotakiwa, lakini haina mamlaka ya kumvua mtu nyadhifa zake isipokuwa Baraza Kuu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, alisema kama Zitto na wenzake wanahisi wameonewa wapeleke hoja yao kwenye vikao vya ndani vya chama.

“Taratibu ziko nyingi, wanazijua, wazifuate, uamuzi ule ni wa Kamati Kuu, si uamuzi wa Katibu Mkuu wala mtu mwingine.

“Katibu Mkuu si kazi yake kuzungumza mambo ya nidhamu kwenye vyombo vya habari, mambo hayo yana sehemu yake, nikiambiwa peleka taarifa hii kwa vyombo vya habari nitafanya hivyo, lakini taarifa ile ni tangazo la Kamati Kuu, si la Dk. Slaa,” alisema Dk. Slaa.

Uamuzi wa kuwavua nyadhifa zao zote katika chama, ulifikiwa na Kamati Kuu, mwishoni mwa wiki iliyopita, katika kikao chake cha siku mbili jijini Dar es Salaam.

Zitto na wenzake walidaiwa kuunda kikundi kilichoshiriki kuandaa waraka huo wa mabadiliko yenye lengo la kufanya mapinduzi yasiyo halali ndani ya chama hicho.

Siku mbili baadaye, Zitto na Dk. Kitila juzi walizungumza na waandishi wa habari na kusema Kamati Kuu haikuwatendea haki na hawako tayari kuondoka Chadema.

Zitto, alisema mapambano yaliyoanza ni kati ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa za majitaka.

Naye Dk. Kitila alikiri kuanda waraka unaosema “Mkakati wa Ushindi 2013” na kusisitiza kuwa Zitto hakuhusika na uandaaji wake.
 
RAI:
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top