Televisheni 4K Ultra HD au 4K TV, au akama Sony wanavyoziita 4K UHD TV zimekuwa madukani kwa muda wa mwaka sasa, lakini tunaweza kusema kwamba zilikuwa hazina matumizi, hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna maudhui (content)ya kutosha ya kiwango cha 4K. Lakini kwa wale ambao usawa (fedha) sio tatizo, hili linakaribia kutoweka kwa vile kuna maudhui (content) ya aina mbali mbali yenye ubora wa kiwango cha 4K. Kwenye makala hii tutatoa baadhi ya muongozo juu ya jinsi ya kupata maudhui mbali mbali ya 4K au Ultra HD ili kuipa matumizi yanayostahiki telelvisheni. Lengo hasa la makala hii ni kutoa mwanga ni nani anayestahiki kununua televisheni hizi. Pia tutazungumzia wale wasiostahiki kununua televisheni hizi.

Simu Zenye Kamera za 4K
Kamera kwa siku hizi tunatumia za aina mbili, na wengi moja tu, aina ya kwanza ni ile ya kwenye simu na ya pili ni kamera halisi kwa matukio maalum. Kwa upande wa simu kuna simu kadhaa kwa sasa zenye uwezo wa kurekodi video za 4K, miongoni mwa zimu hizo ni Acer Liquid S2 na Samsung Galaxy Note 3. Simu zote hizi zinarekodi video za 4K kwa yiho zinaweza kuwa suluhisho la ukosefu wa maudhui (content) kwa atakayeamua kununua TV hizi, kwa upande wa kurekodi video binafsi. Simu hizi zinagharimu baina ya £500 na £650 (Bei za UK)

Kamera na Kamkoda za 4K
Unapotaka kamera hasa (professional) basi Black Magic Cinema Camera ni suluhisho zuri kwani kamera hiyo ina uwezo wa rezolushani 2432 x 1366 ambazo zaidi ya HD. Bei ya kamera hii ni kiasi cha $1600 (bei ya US) Pia kwa upande wa kamkoda kamili kuna nyingi mbali mbali kwa ajili ya matukio muhimu badala ya matumizi ya kila siku. Miongoni mwa kamkoda za Ultra HD ni pamoja na Sony FDR-AX1 ambayo rezolushani unapochukua video huwa mpaka 3840 x 2160 yaani mara mbili ya full HD 1080p. Hapa itabidi ucheue karibu $3,800 (Bei ya US)


Matangazo ya Vipindi ya 4K
Hata hivyo sehemu muhimu ya maudhui ni movie na matangazo ya vipindi (broadcasters). Kwa upande wa vipindi mbali mbali vya kila siku ukiwemo mpira wa miguu wakazi wa Uingereza watarajie karibuni hivi Sky watatoa boksi la TV lenye kuonyesha katika kiwango cha 4K ambalo tayari boksi hilo liko majaribioni. Tegemea kulipia zaidi ya £70 kwa mwezi kwani Sky World ambayo ina Ful HD na 3D tayari inagharimu zaidi ya £60 kwa mwezi. Ingawa bei hii huenda ikashuka baada ya muda mfupi au Sky ikatumia boksi hili kama njia ya kuvutia wateja zaidi kwa kutopandisha bei kabisa.

Media Player za 4K
Sony 4K Ultra HD Media Player ndio kitumbuizo cha movie kwa bei angalau tunaweza kuiita nafuu sana katika anga hizi. Media player hii inagharimu $700 na unaruhusiswa kustream na kupakua movie kwa idadi yoyote unayoitaka kuanzia utakapolinunua bila ya malipo ya mwezi. Hata hivyo Sony 4K Ultra HD Media Player kwa sasa lin a4K movie 70 tu, hata hivyo Sony bado wanaliongezea Box hilo movie zaidi. Cha msingi ni kwamba kasi yako ya inteneti iwe kubwa mno unapoamua kutumia boksi hili.

Nani asiyestahiki Kununua 4K TV
Jambo la kuzingatia ni kuwa ikiwa huna njia ya kupata maudhui (content) yenye kiwango cha 4K au UHD, kununua televisheni ya 4K UHD TV ni uamuzi ambao hauna busara kwa sababu zifuatazo:
  • Kupoteza pesa kwa vile utakaposubiri miezi kadhaa televisheni hizi zitashuka bei kwa kiasi kikubwa ambapo kwa sasa zinapatika kwa zaidi ya $5000.
  • Pia TV hiyo itakuwa haina faida kwa vile utaishia kuangalia maudhui yenye kiwango cha HD au hata chini ya hapi. Hii ina maana wewe na yule atakayenunua HD TV hamna tofauti yoyote kwa upande wa viwango vya ubora wa picha mnazoangalia.
  • Kusubira kwa upande mwengine ni bora zaidi kwa vile mbali na kuteremka kwa bei kila unavyozidi kusubiri basi ubora wa TV hizi unaongezeka, kwa mfano watu walionunua mwanzoni kabisa wanatofauti kubwa na watu watakaonunua katika miezi hii kwa vile wanunuaji wa sasa hivi wana chaguo la skrini mbonyeo (curved screen)
Jambo la msingi zaidi ni kwamba kwa wale tunaoishi Tanzania, Kenya, Uganda au nyingi miongoni mwa nchi za Afrika bado  hatuna sababu ya kununua 4K TV.  Hasa tukizingatia kuwa matangazo ya televisheni mengi bado hayana kiwango halisi cha 1080p HD seuze 4K ambayo kiubora yana kiwango cha ubora mara nne ya HD. 
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top