Kama ulidhani Samsung Galaxy S4 ndio kali ya mwaka kutoka Samsung basi kaa mkao wa kula, Samsung wametangaza TV ya S9 kuwa itauzwa madukani mwaka huu. TV hiyo ambayo ni 4K Ultra HD ina rezolushani mara nne kuliko Televisheni za HD za kawaida. Yaani mn’gao na uzuri wa skrini ya TV hii jicho la mwanadamu halina uwezo wa kuuona kwa ukamilifu wake. Samsung wamesema kwamba televisheni hiyo itauzwa kwa TSh 64,539,029.98 (US$ 40,000), Samsung inaanza kupokea oda za televisheni hii kuanzia mwezi huu. 

Kabla hatujaendelea kwanza tuweke wazi kwamba hii sio televisheni iliyoghali kuliko zote Duniani, na wala haikaribii kabisa kulitwaa taji la ughali katika viwanja vya bidhaa hii. Samsung S9 ambayo ilikuwepo kwa uzinduzi kwenye maonyesho ya Consumer Electronic Show (CES) huko Las Vegas ina ukubwa wa inchi 85. Yaani ukisimama mbele na karibu ya TV hii ni kama vile umekabiliana na ukuta kwa ukubwa. 


Mbali na ukubwa na uzuri wa skrini, TV hii pia ina teknolojia ya 3D Active shutter, teknolijia ambayo wengi miongoni mwa watumiaji wa 3D hupendelea mbadala yake ambayo ni Passive, japokuwa Active ina uzuri wake, kikubwa ni kwamba miwani zake ni lazima utumie zile zile za Samsung wakati passive unaweza tu kutumia hata miwani za sinema ambazo huuzwa kwa bei rahisi mno ukilinganisha na zile za aina ya active shutter.

Aina ya kioo kilichotumiaka kwenye TV hizi ni OLED.  Pia spika zake zinatoa jumla ya watts 120. Ingawa hata TV za kawaida (HD) za Samsung zina apps, kwenye TV hii Samsung wanadhamiria kuwa na apps za ziada zitakazokuwa na mambo ambayo hayatapatikana katika TV hizi za milioni chache tulizozizoea. 

TV inayoongoza kwa ughali zaidi (kwa tulizozipitia) ambayo bei yake ni mara 12 ya Samsung ni Panasonic TH-152UX1 3D 4K2K HDTV ambayo ina ukubwa wa inchi 152 na bei yake ni karibu Dola Nusu milioni ($ 480,000) ambayo ni sawa na TSh. 774,468,359.74. 

Pia kwa mtazamo wetu Samsung wameiuza TV hii bei ghali sana kwa vile Sony na LG nao wametoa televisheni za 4K Ultra HD zikiwa na ukubwa na teknolojia zinazofanana na Samsung hii lakini zinauzwa karibu nusu ya bei ya Samsung S9. 
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top