DAR ES SALAAM. MTANGAZAJI wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi, amefanya ibada na kusema: “Namshukuru Mungu kwa kumponya.”
Ni mara ya kwanza Saro kuzungumza tukio hilo tangu
aliporuhusiwa kutoka Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu, MOI ya
Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa.
Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la
Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba, Jimbo la Magharibi, Ufoo
huku akitokwa na machozi na wakati mwingine kushindwa kuzungumza
alisema: “Ni miujiza tu ya Mungu yeye kunifanya mimi kuwa hai leo.”
Mtangazaji huyo ambaye alilazwa kwa zaidi ya wiki
mbili, aliwashukuru watu wote waliomtia moyo, kumsaidia kipindi chote
alichokuwa mgonjwa.
“Sina cha kuwalipa, ninawashukuru sana kwa wema
wenu, pia kwa kuniombea. Mungu ni mkubwa na amenipigania, naendelea
vizuri kwa sasa,” alisema na kuongeza:
“Mungu alinisimamia na nyinyi pia mliniombea,
hakika sina budi kushukuru kwa kila jambo. Nitasoma zaburi ya 146 katika
Biblia Takatifu ili kumshukuru Mungu kwa kunisaidia.”
Ufoo alisema kuwa ameamua kumshukuru Mungu kwa sababu siyo watu wote wanaopata matatizo kama yake wanapona.
Mchungaji aliyeongoza misa hiyo iliyoanza saa 4
asubuhi hadi saa 7 mchana, Joseph Maseghe alisema Mungu hakupanga Ufoo
afariki dunia kwa kupigwa risasi.
“Mungu bado anakuhitaji, hakupanga ndiyo maana upo
nasi leo. Hautakiwi kulia huu ni mwanzo wa maisha yako mengine, usilie
unachotakiwa ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema.
Misa hiyo ilihudhuliwa na watu mbalimbali wakiwamo
wafanyakazi wa ITV pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace
Kihwelu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John
Heche.
Baada ya kumalizika kwa misa hiyo, ndugu na
marafiki wa karibu wa Ufoo walialikwa na mtangazaji huyo katika hafla
fupi ya chakula cha mchana.
Akizungumza wakati akiwakaribisha wageni katika
chakula cha mchana, alisema: “Nimepata pigo kubwa katika maisha yangu,
familia yetu sasa haina baba wala mama, kweli namshukuru Mungu na
nawaombea kwa Mungu wote walioniombea na kunitakia mema, sijui nimpe
nini Mungu, sijui kwa kweli.”MWANANCHI.