P-Square. |
Uuzwaji wa tiketi za tamasha la kundi maarufu zaidi la muziki wa kizazi kipya barani Afrika, P-Square, umeanza kufanyika jijini Dar es salaam ambapo zitauzwa kwa awamu tatu kwa bei tatu tofauti.
Wadhamini wakuu wa tamasha hilo, kampuni ya simu ya VodacomTanzania, wamekuwa wa kwanza kuuza tiketi hizo ambapo kupitia M-pesa wanauza tiketi kwa shilingi 30,000, zoezi litakalodumu hadi tarehe 17 mwezi huu.
Akiongea na gazeti hili, Alex Galinoma, Afisa masoko wa kituo cha EATV, amesema baada ya tarehe 17 tiketi zitapanda bei na kuuzwa shilingi 35,000ambapo safari hii zitakuwa zikiuzwa kwenye maduka mbali mbali jijini Dar es salaam ambayo yatatangazwa.
"Bei hii itaendelea mpaka mchana wa siku wa tamasha ambapo sasa, ukienda eneo la tamasha(Leaders Club) kununua tiketi mlangoni zitakuwa zikiuzwa shilingi 50,000, alifafanua Galinoma.
Mara ya mwisho kundi hilo lilipokuja jijini Dar, walikuja kwenye tamasha liloandaliwa na kituo cha EATV, tamasha hilo lilipewa jina la kibao chao kilichokuwa kikitamba wakati huo "Do Me".
Katika tamasha hilo lililofanyika Agost 31, mwaka 2008, katika viwanja vya Leaders Club, kiingilio kilikuwa ni 20,000 ambapo walifanya onyesho la dakika 45 huku wakitumia mtindo wa Playback.
Kwa mujibu wa Galinoma, safari hii wanamuziki hao watakuja na bendi nzima na watatumia mtindo wa ala na watakuwa jukwaani kwa masaa mawili bila kupumzika.
Galinoma alisema tamasha hilo la P-Square litaanza rasmi kuanzia saa moja jioni mpaka saa 7 usiku, ili kuwapa mashabiki muda wa kupumzika na kuendelea na mambo mengine.
Milango ya Leaders club itakuwa wazi kuanzia saa 12 jioni na mashabiki wataweza kuingia. Washabiki wanashauriwa kufika mapema Leaders club kwa sababu kutakuwa na ukaguzi wa kutosha na ulinzi mkubwa kwenye tamasha hili.