Tukio hilo limemkosesha nafasi ya kupata haki yake ya msingi, elimu. Emma katika maelezo yake anasema elimu ndio ingemsaidia katika maisha yake yeye na mwanae. Akiwa na namba yake ya mtihani tayari kwa ajili ya kufanya mtihani wa kidato cha nne 2013, Emma alisubiria kwa hamu majibu ya ombi lake kwa Wizara ya Elimu imruhusu kufanya mtihani huo. Hata hivyo, Emma hakuweza tena kufanya mtihani kwa kuwa hakupewa ruhusa ya kufanya hivyo.
Kupitia Wanawake Live, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe amezungumza na kueleza sheria ikoje katika masuala kama haya, na kumalizia kuwa ‘Hakuna mimba za bahati mbaya’. Maswali ambayo wengi wanajiuliza ni pamoja na Je, sheria inayotumika kuongoza elimu nchini Tanzania, inawanufaisha wananchi au ni sheria iliyowekwa kukandamiza kikundi fulani cha watu? Je, Emma Roberts hakupaswa kupigania haki yake ya kupata elimu eti kwa sababu Waziri wa Sheria na Katiba amesema kwamba ‘Hakuna mimba za bahati mbaya’?
Mara zote jamii imeshuhudia wasichana wadogo wakifukuzwa shule kutokana na tatizo la mimba, bila kutazama chanzo cha mwanafunzi huyo kupata hiyo mimba. Pia, wahusika wakuu wa mimba hizo (wanaume) wengi wamethibitika kuendelea kupeta tu mtaani bila kuchukuliwa hatua zozote ilhali msichana anakuwa ameshafukuzwa shule na kunyimwa haki yake ya kimsingi. Muda umefika sasa wanawake kupigania haki zao dhidi ya sheria kandamizi ambazo zinawanyima fursa muhimu katika maisha. Pia, mawazo mgando kama ya Chikawe eti ‘hakuna mimba za bahati mbaya’ ni kitu kinachopaswa kupigwa vita vikali.