Miaka kadhaa ya nyuma kupitia kona hii niliwahi kuhoji  umuhimu wa mtu kuingia na simu ya mkononi katika nyumba za ibada bila ya kuizima, na hii ilitokana na kitendo cha jamaa mmoja ambaye akiwa katikati ya sala katika Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay, simu yake ilipopigwa kana kwamba yupo baa au grosari bila wasiwasi wowote aliipokea na kuanza kubwabwaja bila ya kujali lolote, hivyo mbali ya kitendo hicho kuonyesha jinsi gani jamaa huyo alivyokosa adabu ndani ya nyumba ya ibada, pia kitendo hicho kilikuwa ni  kero kubwa kwa waumini wengine hapo kanisani.
 Katika kile kinachoendelea kuonyesha kuwa watu wengine bado ni malimbukeni wa kutupa wanapokuwa na simu zao za mikononi, siku chache zilizopita  jamaa fulani nao walisababisha usumbufu na kero kwa watu wengine waliokuwa katika misa ya kumuombea marehemu kabla ya mazishi kwa jinsi walivyozitumia simu zao bila ya kujali kuwa walikuwa wakiwakwaza watu wengine pamoja na mchungaji katika shughuli nzima ya mazishi.
 Hatukatai, katika pilikapilika za kupeana taarifa za misiba pamoja na shughuli nzima zinazohusu mazishi, simu huwa ni mojawapo ya chombo muhimu sana kwa kuwezesha ufanisi  wa mawasiliano, lakini sidhani kama hata kama kuna umuhimu wa aina gani juu ya kupashana habari, basi huyo mtu anayejiona ana umuhimu huo aingie na simu kanisani au msikitini akiwa ameiacha  kengere ya simu hiyo katika sauti ya juu na punde baada ya kupigiwa anaanza kuongea akiwa humo ndani ya nyumba ya ibada!
 Binafsi nahoji, kama mtu unajijua kuwa una umuhimu wa kuendelea kuwasiliana na watu wengine hadi muda wa kuingia kanisani unapowadia, kwa nini usiendelee kuwasiliana na hao watu wako ukiwa nje ya kanisa badala ya kuingia kanisani na kuanza kusumbua watu wengine ambao wanajua fika nini maana ya kuingia kanisani na kitu gani kinaendelea wakati huo.
 Katika hali iliyoonyesha kuwa ustaarabu kwa baadhi ya watu wanapokuwa na simu za mikononi ni mdogo, mbali ya baadhi yao kusumbua kwa milio ya juu ya simu zao hatua iliyomlazimu hadi mchungaji kuomba wale wote waliojisahau kuzima au kuziondolea milio simu zao anawaomba wafanye hivyo ili kuondoa usumbufu utakaosababisha hali ya usikivu kutoweka hapo kanisani, lakini baadhi ya watu hao walionekana kutokuzingatia ushauri huo na kuendelea kusumbua kwa milio ya kengere za simu zao huku misa ikiendelea!
 Hali hiyo ya usumbufu wa simu haikuishia hapo kanisani, ilijitokeza tena tulipofika makaburini, bila aibu jamaa mmoja kati ya wale wale waliokuwa bize na simu zao muda wote wa mahubiri kanisani, wakati ndugu, jamaa, marafiki pamoja na waombolezaji wote wakiwa katikati ya shughuli  za mazishi, jamaa huyo ambaye alisimama karibu kabisa na mchungaji wakati akiongoza shughuli za mazishi, baada ya kupigiwa simu akainyanyua, akageuka nyuma, akaipokea na kuanza kupayuka: “ooh, ongeza sauti, sikusikii, sikusikii…”, hali ambayo ilimlazimu mchungaji anyamaze na kumsubiri jamaa huyo amalize kwanza maongezi yake ndipo aendelee na taratibu za kuongoza mazishi!
 Kwa ujumla kitendo hicho kilionekana kuwakera watu wengi pale makaburini, lakini kutokana na busara za mchungaji, waombolezaji wote kwa ujumla wakatulia na kuendelea na taratibu za mazishi japokuwa baada ya shughuli ya mazishi kukamilika, jamaa huyo alishambuliwa sana kwa kila aina ya maneno anayostahili kupewa mpuuzi mwingine yeyote na umati ule ulioonekana kukerwa sana na kitendo hicho.
 Jamani hivi kweli hata kama mtu una umuhimu wa kuwa na mawasiliano wakati wote, ni mawasiliano ya aina gani hayo ambayo huwezi kujivuta hadi sehemu ya mbali kidogo ili pale utakapokuwa unazungumza na huyo aliyekupigia  usiwakwaze wengine kama jamaa huyo alivyosababisha kero!
 Na  kama kweli wewe ni mtu muhimu na una mawasiliano muhimu, kwa nini sasa huna simu za kisasa ambazo hazihitaji kupiga mikelele kibao hadi uwasumbue watu wengine? 
 Hayo si mambo, simu zote siku hizi zina mitetemo (vibration), wewe makelele kibao ya  simu yako ya Kichina ndani ya nyumba za ibada na makaburini nani anayataka?
-Tanzania Daima
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top