AKISIKIA muziki unapigwa mahali fulani vinyweleo humsisimka, kichwa hutingishika na kama yuko mahali ambako anaweza kujiachia basi lazima aingie kati kuchangamsha mwili kwa kusakata rhumba.

Haijalishi ni muziki wa aina gani unapigwa wakati huo isipokuwa anachoangalia ni mazingira tu. Ukimpigia Bolingo, R&B, Country, Bongo Fleva zote zitamkuna. Yote kwa yote mwanamuziki anayeikonga roho ya JB duniani kote ni Don Williams.

“Ninapenda kusikiliza na kucheza muziki, lakini inategemea wakati huo nipo kama nani, nikiwa kama JB yaani mwigizaji kuna aina ya muziki huwa napendelea halikadhalika nikiwa Jacob,” anasema JB.

Anasema kutokana na kazi yake amejikuta akizijua aina nyingi za muziki na kujiongezea orodha ya nyimbo katika maktaba yake, lakini hii haijambadilisha kuwa yule mtu wa kawaida mwenye chaguo la kipekee.

“Unaniona kwenye majukwaa ya muziki, kumbi za starehe na kwingineko nikijirusha vilivyo, lakini huyo ni JB na si Jacob, Jacob anaenda kanisani na kucheza nyimbo za Injili,” anasema JB.

JB anasema yeye ni mlokole, hivyo katika maisha ya kawaida hupendelea kusikiliza nyimbo za Injili kwa kuwa ndivyo imani yake inavyomruhusu.

“Nimeokoka, mara nyingi huwa ninasikiliza nyimbo za Injili, lakini kwa sababu ninapenda aina nyingine ya muziki huwa ninasikiliza zile ambazo zina mafundisho,” anasema JB.

Anasema mbali na kusikiliza nyimbo za Injili, huwa anapenda kuwasikiliza wanamuziki kama Jose Chameleon, Ben Pol, Profesa Jay, Lady Jay Dee, Twanga Pepeta na wengineo wa nyimbo za kidunia.

“Ninapenda sana muziki, maisha yangu yametawaliwa na kusikiliza au hata kucheza pale ninapopata nafasi iwe nyumbani, kanisani hata kwenye hadhira,” anasema.

Anasema pamoja na kuwa huonekana katika kumbi za starehe na klabu za usiku, haimaanishi kuwa anakwenda huko kucheza muziki bali hufanya hivyo kujifunza mambo mbalimbali.

“Kama utakumbuka kabla ya kutengeneza filamu yangu ya ‘Senior Bachelor’, nilikuwa naenda sana klabu, sikwenda kule kufuata muziki ingawa kiukweli nilikuwa nafurahia, lengo langu lilikuwa kujifunza namna mapedeshee na madj wanavyojirusha ili niweze kuicheza nafasi hiyo vizuri,” anasema JB.

Akizungumzia ujio wake mpya katika filamu, mwigizaji huyo amesema yupo mbioni kuachia kazi mfululizo huku akisisitiza kuwa filamu yake mpya aliyoshirikisha mwanamitindo, Jokate Mwegelo, itatoka baada ya miezi sita.

“Napigiwa simu nyingi, kila mtu anataka kuiona filamu aliyocheza Jokate, lakini siwezi kuitoa mpaka mwezi wa nne mwakani kwani nina kazi nyingi ambazo inabidi zitoke kwanza,” anasema.

Akizungumzia sababu za kumshirikisha Jokate katika filamu hiyo iliyopewa jina la ‘Mikono Salama’, anasema ni kutokana na umbo lake ambalo lilionekana kuwa lingefaa katika nafasi hiyo.

“Unajua Jokate ana kaumbo fulani kazuri ambako unaweza kukachezesha nafasi yoyote, wasanii wengi wamezeeka kuna nafasi huwezi kuwachezesha tena,” anamalizia.
SHUKA CHINI KUTOA MAONI YAKO
 
Top