Miongoni
mwa masharti ya Windows 8 ambayo yaliwekwa na Microsoft ni kutoruhusu
tablet zenye rezolushani chini ya 1366 x 768, lengo la Microsoft likiwa
ni kuhakikisha kwamba wanotoa ushindani katika ubora wa tablet. Hii
imesaidia kwa tablet za Windows 8 kuwa nzuri kiasi fulani lakini
Microsoft wamefanya kosa la kimkakati kwani kuna mfumuko mkubwa wa mauzo
ya tablet kati ya7” na 8” kufuatia mafanikio makubwa ya bidhaa kama
vile iPad Mini, Amazon Kindle Fire na Nexus 7. Rezolushani za juu kabisa
katika tablet za 7" ni zile zilizotumika kwenye Kindle Fire HD na Nexus
7 ambazo zote zina 1280 x 800. (216ppi), hizi zimepungua kwa 1.2%
kufikia kiwango ambacho Microsoft walikitaka awali, ambapo iPad Mini
ina 1024x768 (163ppi), hivyo kwa viwango vya Micrososft iPad Mini iko chini sana.
Baada ya kugundua kosa
hilo Microsoft wameregeza masharti ya Windows 8 na hivyo kwa sasa tablet
ndogo na za rezolushani za chini zitaruhusiwa. Hivyo tutarajie tableti
ndogo za Windows 8 kwenye robo ya mwisho ya mwaka huu au mapema mwakani.
Extreme Tech wakiripoti taarifa hiyo ya Microsoft wameeleza kwamba
taarifa hiyo imefuatiwa marekebisho katika taratibu na sheria za
kuruhusiwa (Certification rules) kutumia Windows 8, hata hivyo hii
itakuwa kwa tolewa la Windows 8 RT peke yake. Faida kubwa ya udogo huu
ni urahisi wa bei. Hata hivyo tablet hizi zitatumia Windows RT tu na
hakutakuwa za Windows Pro, kitu ambacho hakiingia akilini kwa vile cha
msingi ni nguvu ya tablet na si ukubwa wa tablet.
Kwa msingi huu Microsoft bado wanaonekana wamechanganyikiwa na hivyo kujiwekea vikwazo vya kimaendeleo wenyewe. Baada
ya ukiritimba wa muda mrefu kibiashara kwa sasa Microsoft hawako katika
hali nzuri, hii ikiwa ni pamoja na kufanya jitihada kubwa za kuleta
mabadiliko katika bidhaa muhimu za kampuni hiyo na hasa OS za kompyuta,
tablet na simu. Hisa za Windows Phone kulinganisha na OS nyingine ni 6%
kwa mujibu wa repoti ya Mintel, hisa ya Windows 8 katika soko la tablet
kwa mujibu wa ripoti ya IDC ni 2%, mauzo ya PC yanaendelea kuzorota
mwaka hadi mwaka.
Hata hivyo Microsoft
wako mbali na kukata tamaa na hasa katika simu na tableti, hivi karibuni
wamefanya uboreshaji wa Windows 8 na programu kama vile za Mail, People
na Kalenda zimepata sura mpya, pia jarida la Tech linalotolewa na T3
limeripoti kwamba Microsoft wako jikoni wakitayarisha Windows mpya
ambayo imepewa jina la muda (codename) Windows Blue, Windows hii huenda
ni sehemu ya mpango wa Microsoft wa kuziunganisha Windows Phone 8,
Windows RT na Windows 8 Pro kuwa moja na pia kujitayarisha katika wakati
wa kuachana na PC.
Darrell Etherington wa
Tech Crunch akizungumzia Windows Blue baada ya kuijaribu ameonekana
kuvutiwa mno na alichokiona, amesema “Microsoft inaelekea kutumia uzoefu
wake wa UI mpya kuachana na mtindo wa kizamani wa desktop.” Windows
Blue tayari umeshavuja na kujaribiwa na watu kadhaa, naye Paul Thurrott
wa mtandao wa WinSuperSite amesema apps za Windows Blue zinathibitisha
kwamba Windows inaachana na masuala wa desktop ambapo yeye anaamini
kwamba Windows Blue hatimae ndio itakuja kuwa Windows 9.
Ni mapema mno kuanza
kuzungumzia Windows nyingine kwa vile Windows 8 bado ni mpya, hata hivyo
Windows 8 inakabiliwa na kukosolewa hapa na pale huku raisi wa Samsung
kitengo cha Memory Chip bwana Jun Dong-soo akiifananisha Windows 8 na
Vista, Vista ni toleo linaloonekana kuwa Windows walikwenda mchomo, na
hivyo haikukaa muda mrefu kabla ya kutoka mpya yake, je Windows
kuharakisha na toleo la Blue kunatokana na kuwa wameshaona matatizo ya
Windows 8? Nivigumu kulipata jibu la swali hili kwa sasa.
Hata hivyo hatuishi tena
katika ulimwengu wa kusubiri miaka 3 kabla ya kutoa toleo jipya la OS.
Apple katika kipindi cha Miaka mitatu iliyopita wametoa matoleo matatu
tofauti ya Mac OSX yaani Snow Leopard, Lion na Mountain Lion. Nazo OS na
simu na tablet kama vile Android na iOS hutoka toleo jipya karibu kila
mwaka. Hivyo huenda Microsoft wameamka kutoka kwenye usingizi mzito wa
kuacha OS kukaa miaka 3 au zaidi.